Uteuzi wa Jokate Mwegelo UVCCM Waibua Mfarakano
Uteuzi   wa Miss Tanzania namba mbili wa mwaka 2006, Jokate Mwegelo kuwa Kaimu  Katibu wa Uhamasishaji wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM)  Taifa, unaonekana kutaka kuivuruga jumuiya hiyo.
Mjadala  mkubwa umeibuka kuhusu uteuzi huo, ambapo baadhi ya wanachama na  viongozi wa juu wa jumuiya hiyo wamedai kuwa haukufuata kanuni na  taratibu za umoja huo.
Vyanzo  vya kuaminika kutoka katika umoja huo vimedai kuwa baadhi ya viongozi  wa juu wa UVCCM hawakushirikishwa katika uteuzi huo uliofanywa na kigogo  mmoja wa umoja huo.
Taarifa  za ndani zinaeleza kuwa uteuzi huo haukushirikisha wajumbe wa Kamati ya  Utekelezaji wala Baraza Kuu la UVCCM, ambalo halikukutana kumthibitisha  Jokate kama kanuni zinavyoelekeza.
Kwa  mujibu wa kanuni za jumuiya hiyo, wajumbe wa kamati ya utekelezaji  hawazidi 10, ambapo miongoni mwao ni Mwenyekiti wa umoja huo Taifa,  Makamu Mwenyekiti Taifa, Katibu Mkuu, Naibu Katibu Mkuu na mjumbe mmoja  kutoka makao makuu ya chama.
Wajumbe wa baraza kuu ni wenyeviti na makatibu wa mikoa na mjumbe mmoja kutoka katika kila mkoa.
Kutokana  na kile kilichodaiwa kuwa ni mvurugano ndani ya umoja huo, Kaimu Katibu  Mkuu wa UVCCM Taifa, Shaka Hamdu Shaka, amesema kuwa uteuzi huo  ulifuata taratibu zote za chama.
“Ni  kweli amekaimishwa kwa kufuata taratibu zote za chama, kikao cha Kamati  ya Utekelezaji kilikutana Aprili 18, mwaka huu, Dar es Salaam na ndicho  kimewakaimisha wakuu wa idara watano akiwamo Jokate.
“Hao  wanaolalamika hawajui kanuni na taratibu za jumuiya yetu, huwezi kupata  nafasi kama kikao cha Kamati ya Utekelezaji hakijakaa,” alisema Shaka.
Hata  hivyo alikiri kutoitishwa kwa kikao cha Baraza Kuu ili kuthibitisha  uteuzi huo, akisema ni gharama kubwa kuitisha kikao hicho.
“Kwa  kawaida Baraza Kuu huwa linakutana kila baada ya mwaka mmoja, kuita  baraza kuu ni gharama sana hivyo ikitokea kuna nafasi wazi Kamati ya  Utekelezaji ina mamlaka pia ya kumthibitisha,” alisema.
Kwa upande wake, Jokate alishukuru kwa uteuzi huo na kuahidi kuifanya jumuiya hiyo iwe karibu zaidi na vijana wa Kitanzania.
“Nashukuru  kwa imani waliyoonyesha viongozi wangu ila zaidi kuona nina uwezo wa  kuongoza idara hiyo nyeti na muhimu kwenye jumuiya.
“Kikubwa  ni kuifanya jumuiya iwe karibu zaidi na vijana wa Kitanzania na  kurudisha tumaini na kusimamia changamoto wanazozikabili vijana katika  kujiletea maendeleo,” alisema Jokate.
Jokate  pia alikuwa miongozi mwa wanachama 450 wa CCM waliojitokeza kuchukua  fomu za kuwania ubunge wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA).
Jokate alianzia kwenye mashindano ya Miss Tanzania mwaka 2006 ambapo aliibuka mshindi wa pili.
Hivi  sasa anajishughulisha na sanaa na ujasiriamali ambapo anamiliki Lebo ya  Kidoti Fashion inayojihusisha na uuzaji wa nywele na mavazi. 

No comments