Mgogo CUF Wazidi Kuwaka Moto......Wabunge Walaani, Polisi Wafuta Mkutano wa Maalim Seif
Siku   moja baada ya kutokea kwa vurugu kubwa katika mkutano wa viongozi wa  Chama cha Wananchi (CUF) Wilaya ya Kinondoni, Dar es Salaam kwa kuvamiwa  na genge la watu waliokuwa na silaha za moto, wabunge wa upinzani  wameibuka na kuitupia lawama Serikali.
Kutokana  na hali hiyo wabunge hao wamesema ukimya wa Serikali kuhusu uvamizi huo  wa viongozi wa CUF, huku wakitangaza kumwandikia barua Mkuu wa Jeshi la  Polisi (IGP), Ernest Mangu pamoja na taasisi nyingine za Serikali  kuhusu tukio hilo.
Akizungumza  na waandishi wa habari mjini Dodoma, Naibu Mnadhimu wa Kambi rasmi ya  Upinzani bungeni, Ally Saleh alishangazwa na ukimya wa Waziri wa Habari,  Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe kwa kushindwa  kujitokeza na kukemea hatua ya waandishi wa habari kupigwa katika  mkutano huo.
Kutokana  na hilo, wamelaani kitendo hicho cha uvamizi wa mkutano pamoja na  waandishi wa habari kupigwa huku wakiitaka Serikali kutoa tamko na  kuchukua hatua kali dhidi ya waliohusika.
Wakati wabunge hao wakitoa tamko hilo,  Dk. Mwakyembe  yeye amekana kuwa taarifa juu ya tukio hilo. 
“Mimi  sijui chochote ndiyo nasikia kwako, kwani hao wabunge wamekwambia kama  wameniletea taarifa hizo? Mimi niko Dodoma…sifahamu chochote,” alisema.
Akizungumzia  hali hiyo Saleh, alisema chama cha CUF, kimeshamwandikia barua IGP  Mangu pamoja na taasisi nyingine za Serikali kuhusu tukio hilo.
Alisema  ukimya wa Waziri wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba na Dk. Mwakyembe  juu ya tukio hilo umeonesha kuwa hawajatimizi majukumu yao ipasavyo.
 “Mambo haya yanavyotokea mawaziri wawili tunataka kuwavisha mnyororo, Waziri Mwigulu Nchemba na Mwakyembe.
“Mwakyembe  alipaswa kujitokeza kwa haraka na kutoa tamko, tunahisi jukumu la  Serikali halijatekelezwa, Mwakyembe anapaswa kuhakikisha usalama wa  waandishi unakuwapo,” alisema.
Saleh  ambaye ni Mbunge wa Malindi alisema kikundi cha ‘Mungiki’ si kigeni  hapa nchini na Serikali inakifahamu lakini hakuna hatua zozote ambazo  zimeshachukuliwa hadi sasa.
Aidha  alisema kutokana na tukio lililotokea juzi, ziara  iliyokuwa ifanywe na  Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Shariff Hamad upande wa bara jana  ilifutwa na Serikali.
“Kitendo  cha Serikali kuufuta mkutano huo si sawa kwa sababu bwana yule (Profesa  Ibrahim Lipumba) anabebwa na mbereko ya Serikali kwa kufanya mikutano  ya ndani kila wakati.
“Serikali  inalea Jamhuri ndogo ndani ya Jamhuri, vile vile Serikali imekuwa  inalea kambi ndogo ndani ya Buguruni na kwamba wanufaika zaidi wa  mgogoro unaoendelea ndani ya CUF ni Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambao  dhumuni lao ni kuchukua majimbo yanayoongozwa na CUF katika uchaguzi  mkuu ujao,”alisema.
Kwa  upande wake Naibu Waziri Kivuli wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa  na Michezo, Devotha Minja alisema matukio wanayofanyiwa waandishi wa  habari yanapaswa kukemewa.
“Waandishi  wa habari ni kiungo cha serikali na wananchi, pia ni kiungo kati ya  wanasiasa na wananchi, suala walilofanyiwa jana linapaswa kukemewa na  halipaswi kuendelea kutokea,” alisema Minja.
Minja  ambaye pia ni Mbunge wa Viti Maalumu (Chadema), alisema waandishi wa  habari wamekuwa wakionewa na kupigwa, akitolea mfano wa tukio la  kuvamiwa kwa Kituo cha Televisheni cha Clouds, kutekwa na kuteswa kwa  Absalom Kibanda, kuuawa kwa aliyekuwa mwandishi wa Channel Ten, Daud  Mwangosi.
Kutokana  na vurugu hizo ambazo zilisababisha mtu mmija anayedaiwa kuvamia  mkutano huo kujeruhiwa,  Jeshi la Polisi limesema bado linaendelea na  uchunguzi wa kina kuhusu tukio hilo na hadi sasa hakuna mtu yeyote  anayeshikilia.
Kamanda  wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, Suzan Kaganda, amesema bado  wanaendelea na uchunguzi wa tukio hilo ikiwa ni pamoja na wahusika  waliosababisha vurugu hizo.
“  Kwa sasa hatuwezi kuzungumzia jambo lolote kuhusu tukio  hilo…tunaendelea na uchunguzi wa kina kuhusu vurugu hizo na baada ya  uchunguzi wetu kukamilika tutatoa taarifa ,”alisema Suzan. 

No comments