Tamko la serikali kuhusu kushambuliwa waandishi wa habari katika mkutano wa CUF
Serikali  imepokea kwa masikitiko taarifa za kushambuliwa na kujeruhiwa baadhi ya  waandishi wa habari katika mvutano uliotokea juzi jijini Dar es Salaam  kati ya wafuasi wa pande mbili zinazokinzana za Chama cha Wananchi  (CUF). Tumechukua muda kidogo kulifuatilia suala hili na kubaini licha  ya baadhi yao kujeruhiwa na kuripoti polisi, wapo waandishi ambao vifaa  vyao vya kazi pia vililengwa katika shambulizi hilo.
Tunachukua  fursa hii kulaani kitendo cha kuumizwa wanahabari tena waliokuwa  wamealikwa kuhudhuria mkutano huo. Ifahamike kuwa uandishi wa habari ni  taaluma adhimu na nadhifu inayopaswa kuheshimiwa, kuenziwa, kulindwa na  kutoingizwa katika migogoro ya pande zinazofarakana katika jamii.
Kifungu  cha 7 (1) (a) cha Sheria ya Huduma za Habari Na. 12 ya mwaka 2016  kinaainisha uhuru wa wanahabari katika kukusanya habari kwa muktadha wa  kuwepo katika maeneo ya matukio kama hakuna sababu nyingine za kuzuiwa.  Misingi ya uhuru huu wa kitaaluma pia imesisitizwa katika Ibara za 18 ya  Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 1977 na 19 ya Mkataba wa  Kimataifa wa Haki za Kiraia na Kisiasa wa mwaka 1966 ambao nchi yetu  imeuridhia.
Tunawatakia  nafuu ya haraka wanahabari waliojeruhiwa na wenzao wengine waliopatwa  na jakamoyo katika tukio hilo. Kwa kuwa suala hili tayari limeripotiwa  polisi, tunawaomba wadau wote wa habari na wanasiasa kwa sasa kutulia na  kuviachia vyombo husika vilifanyie kazi ili hatua stahiki za kisheria  zichukuliwe.
Imetolewa na:
Dkt. Hassan Abbasi
Mkurugenzi, Idara ya Habari-MAELEZO na Msemaji Mkuu wa Serikali


No comments