Polepole Aitaka CCM Imchukulie Hatua za Kinidhamu Nape Nnauye
Katibu  wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Humphrey Polepole  amelaani vikali kauli iliyotolewa na mtangulizi wake ambaye ni mbunge wa  jimbo la Mtama, Nape Nnauye kuwa alisaidia kukitoa chama hicho shimoni.
Nape  alitoa kauli hiyo dakika chache baada ya mkutano wake na waandishi wa  habari kuzuiwa na kutishiwa bastola na mtu mmoja, siku moja baada ya  kuondolewa kwenye nafasi ya Uwaziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na  Michezo.
Polepole  alisema kuwa kauli hiyo ya Nape sio kauli sahihi ya kiongozi na kwamba  yeye pekee hawezi kukitoa chama shimoni huku kukiwa na wanachama milioni  nane na maelfu ya viongozi.
“Mwanachama  anayejitambua hawezi kusema anakibeba chama, wanachama wote milioni  nane walikuwa wapi? Viongozi wote maelfu walikuwa wapi? Nape ni kiongozi  wetu kwenye chama, kama kweli alisema maneno hayo alikengeuka sana,” Polepole anakaririwa na Mwananchi.
Katibu  huyo wa Itikadi na Uenezi wa CCM alisema kuwa Kamati ya Maadili  inapaswa kuliangalia suala hili na kumchukulia hatua Nape.
“Tuna  kila sababu za kumshauri Mzee Mangula wa Kamati ya maadili kuwa  hatuwezi kuwa na viongozi wa aina hii. Chama chenye watu milioni nane  unakitoa shimoni na nini? Unakitoa na ngazi, ulitumia kamba kukitupia  shimoni, uliita zimamoto? "Alihoji.
Hata  hivyo, Polepole alisema kuwa hatua zinazopaswa kuchukuliwa kwa viongozi  kama Nape sio za kuwawekea ukomo bali kuwalea kimaadili kwa kutumia  hekima na busara ili watambue kuwa chama sio punda anayeweza kutumbukia  shimoni. 
Hivyo, alisema CCM iko kwenye mpango wa kuanzisha chuo kikuu kitakachotoa mafunzo kwa makada wake kuhusu nidhamu na maadili.

No comments