Jeshi la Polisi Lasema Linawashikilia Watu 3 Kwa Kuvamia Mkutano wa CUF na Kuwapiga Watu
Saa   tatu baada ya viongozi wa CUF kukutana na Kamanda wa Polisi wa Kanda  Maalumu ya Dar es Salaam, Simon Sirro, kuhoji sababu za kutokamatwa watu  waliofanya vurugu kwenye mkutano wa waandishi wa habari na viongozi wa  chama hicho wa wilaya ya Kinondoni, Jeshi la Polisi limetangaza  kushikilia watu watatu.
Wakiongozwa  na Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi ya Chama hicho Julius Mtatiro,  viongozi hao waliwaeleza wanahabari kuwa ni ajabu kuona  Polisi  haijachukua hatua huku ikijulikana wazi kuwa watu hao walijeruhi  wanahabari na viongozi wa chama hicho katika tukio ambalo liliripotiwa  na vyombo vya habari.
Viongozi  hao walikutana na Sirro jana saa 5 asubuhi na kuzungumza kwa takribani  saa moja, na kisha saa 8 mchana Kamanda huyo alizungumza na waandishi wa  habari na kueleza kukamatwa kwa watu hao, wakituhumiwa kuhusika katika  tukio hilo.
Jumamosi  iliyopita takribani watu watano wakiwa kwenye gari lenye nembo na  bendera za CUF, walivamia mkutano huo uliokuwa ukifanyika kwenye hoteli  ya Vinna, Mabibo wilayani Kinondoni na kufanya vurugu.
Miongoni  mwa watu hao, mmoja aliyekuwa amejifunika uso kininja alichomoa bastola  na kutishia huku mwingine akishindwa kuondoka baada ya kuachwa na  wenzake, jambo lililosababisha wananchi wamzingire na kumshushia kipigo.
Katika  ufafanuzi wake, Mtatiro alisema tukio hilo ni la 13 dhidi ya upande  unaomwunga mkono Katibu Mkuu wa Chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad  lakini vyombo vya Dola viko kimya.
“Baada ya tukio la juzi (Jumamosi) tulikaa kimya ili kuona kama polisi watasema chochote ila imekuwa tofauti. Wako kimya tu,” alisema Mtatiro.
Akieleza kilichowapeleka kituoni hapo, alisema: “Tulitaka  kujua yule mvamizi aliyekuwa na bastola mpaka sasa yuko wapi. Mvamizi  mmoja tunajua alikamatwa na wananchi, akapigwa kidogo na kuokolewa.  Tulitaka kujua alitoa maelezo gani.”
Alisema  baada ya tukio hilo, Mkuu wa Upelelezi aliwapigia simu viongozi  waliovamiwa akiomba waende kituo cha Polisi Magomeni  wakapatanishwe.
“Tulishangazwa  na taarifa hiyo, kwa watu waliovamiwa kwenda kupatanishwa. Tulijihoji  kama Jeshi la Polisi linaweza kupatanisha watu wenye makosa ya jinai,  kwani mtu wa makosa hayo upelelezi unapokamilika hupelekwa mahakamani,” alisema Mtatiro.
Alisema sababu nyingine ya kwenda kituoni hapo ni kutaka kufahamu kama watu wanaofanya matukio hayo wako juu ya sheria.
“Tulimwonya  Kamanda Sirro kwamba sisi (upande wa Maalim) tuna nguvu kuliko Lipumba  na kuiomba Polisi kutekeleza majukumu yake kwa kuchukua hatua dhidi ya  wavamizi hao,” alisema.
Katika mkutano wake na wanahabari, Sirro alisema Polisi inashikilia watu watatu wakituhumiwa kufanya vurugu kwenye mkutano huo.
“Tulipata  taarifa ya kuvamiwa kwa mkutano wa wanachama wa CUF na watu  wasiofahamika wakiwa na silaha. Baada ya taarifa hizo kupokewa askari  walifuatilia na kukamata watu watatu,” alisema Sirro.
Alisema watuhumiwa hao wanaendelea kuhojiwa na upelelezi ukikamilika hatua za kisheria zitafuatwa.
Alisema hakuna mtu aliye juu ya sheria na kusisitiza kuwa waliohusika watasakwa kokote watakokuwa.

No comments